MyElimu

Full Version: Mmkaidi Na Siku Ya Eid
You're currently viewing a stripped down version of our content. View the full version with proper formatting.
MKAIDI NA SIKU YA EID

Kuitika imebidi, ndo sifa ya muungwana,
Hoja yako sina budi, kuijibu kwa upana,
Kuhusu siku ya eid, nae mkaidi mwana,
Hata mwana mkaidi, siku ya eid hunona.

Mtoto awe kaidi, jeuri anotukana,
Nyumbani huwa harudi, usiku hata mchana,
Vituko vya makusudi, kifupi kashindikana,
Hata mwana mkaidi, siku ya eid hunona.

Awe anaitwa Sudi, Shabani ama Amina,
Pindipo ataporudi, chakula kwake hakuna,
Tena fujo zikizidi, kipigo kwake cha mana,
Hata mwana mkaidi, siku ya eid hunona.

Wazazi wawe baridi, ama ni wakali sana,
Watamuita hasidi, mabaya mengi majina,
Ila ikifika eid, wote hawatomkana,
Hata mwana mkaidi, siku ya eid hunona.

Iwe juisi baridi, na pilau lilonona,
Hata mkono wa eid, na nguo watazishona,
Marashi hata na udi, ili anukie sana,
Hata mwana mkaidi, siku ya eid hunona.

Huyu ndiye mkaidi, wahenga walomuona,
Siku zote hafaidi, hadi eid ikifana,
Nadhani nimeirudi, methali yake maana,
Hata mwana mkaidi, siku ya eid hunona.



Karibu: www.mwalimuwakiswahili.com
Hongera ticha..[img]images/smilies/biggrin.gif[/img]